𝐏𝐄𝐓𝐑𝐎𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐒𝐇𝐔𝐊𝐀, 𝐃𝐈𝐙𝐄𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐏𝐀𝐍𝐃𝐀
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika nchini kuanzia Juni 3, 2026. Katika mabadiliko hayo, bei ya petroli imepungua kwa Sh29 kwa lita, kutoka Sh4,115 hadi Sh4,086 kwa lita. Hata hivyo, bei ya dizeli imeongezeka kwa Sh85 kwa lita na sasa kuuzwa kwa Sh4,333 kutoka Sh4,248 ya mwezi Mei.
EWURA imeeleza kuwa licha ya ongezeko hilo, Serikali imetoa ruzuku ya Sh534 kwa kila lita ya dizeli ili kupunguza athari kwa watumiaji na sekta mbalimbali za uchumi. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Gerald Maganga, amesema mabadiliko hayo yamesababishwa na hali ya machafuko na migogoro inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, jambo lililosababisha kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Kwa ujumla, EWURA imezitaka kampuni zote za mafuta kuzingatia bei kikomo zilizotangazwa na kuonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelekezo hayo.








Maoni
Chapisha Maoni