ACHENI KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI
Na, Mwandishi wetu Shinyanga
Maafisa usafirishaji katika Manispaa ya Shinyanga wamepatiwa elimu ya usalama barabarani kuhusu kuacha tabia ya kujichukulia Sheria mkononi pindi matukio ya ajali yanapotokea badala yake watoe taarifa Kituo Cha Polisi ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Akitoa elimu hiyo katika Stendi kuu ya Mabasi Mkoa wa Shinyanga Askari Polisi wa Kikosi Cha usalama barabarani Mkoa wa Shinyanga Sajenti David Ndimila ambapo amewataka Maafisa usafirishaji hao kuacha kushawishiana kufanya vitendo vinavyopelekea vurugu ikiwa ni pamoja kuchoma moto vyombo vya moto, kujeruhi mhusika kwenye ajali hiyo na kuharibu miundombinu Kwa kufanya hivyo ni kutoa hukumu isiyo halali na ni kinyume na Sheria za Nchi.
Sajenti Ndimila amewaeleza madereva hao kuwa vitendo hivyo wakivifanya vinaweza kusababisha uharibifu, majeruhi au vifo kitu ambacho kinaweza kuwapelekea kuingia kwenye kesi ya jinai pia vitendo hivyo vinaweza kuwageukia wao pindi watakaposababisha ajali Kwa kipindi kingine endapo kama vitaendelea kushamiri.
Aidha Maafisa usafirishaji hao wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kwa kutoa ushahidi kuhusiana na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani pia kuacha tabia ya kuficha vyombo vya moto vilivyohusika kwenye ajali zilizotokea kwani kufanya hivyo ni kujiingiza kwenye vitendo vya kiharifu na kukwamisha upelelezi wa kesi husika.

Kwa ujumla, maafisa usafirishaji wametakiwa kuzingatia sheria za nchi kwa kuepuka kujichukulia sheria mkononi pindi ajali zinapotokea, badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa usahihi na kudumisha amani na usalama wa jamii.



Maoni
Chapisha Maoni