MAMELODI SUNDOWNS MABINGWA (CAF CHAMPIONS 2026)
Miamba ya soka kutoka Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns (Bafana Ba Style), imetawazwa rasmi kuwa Mabingwa wapya wa Afrika baada ya kulazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa pili wa Fainali ya CAF Champions League uliopigwa Jumapili, Mei 24, 2026, kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat.
Kwa sare hiyo, Mamelodi Sundowns inayofundishwa na kocha Miguel Cardoso imetwaa ubingwa huo mkubwa zaidi ngazi ya klabu barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 (aggregate), kufuatia ushindi wao wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld jijini Pretoria.
Dakika 90 za Moto Jijini Rabat:
Katika mchezo huo wa marudiano uliopigwa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wa Morocco, wenyeji AS FAR walikuwa wa kwanza kupata bao la uongozi mnamo dakika ya 40 kupitia mkwaju wa penati uliopigwa kwa usahihi na nahodha wao, Mohamed Hrimat, kufuatia faulu iliyofanywa na Divine Lunga na kuthibitishwa na mtambo wa VAR.
Hata hivyo, furaha ya wenyeji haikudumu kwa muda mrefu kwani kiungo fundi wa kimataifa wa Sundowns, Teboho Mokoena, alisawazisha goli hilo katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza (45+7') kwa shuti kali la kwanza lililogonga mwamba wa juu kabla ya kutinga nyavu, akipokea pasi kutoka kwa Tashreeq Matthews.
Kipindi cha pili kilishuhudia nidhamu kubwa ya ulinzi kutoka kwa safu ya ulinzi ya Mamelodi Sundowns chini ya kipa Ronwen Williams aliyekuwa imara kuzuia mashambulizi ya hatari ya AS FAR yaliyokuwa yakielekezwa golini kwake.
Kwa ujumla, Huu unakuwa ubingwa wa pili wa kihistoria wa CAF Champions League kwa klabu ya Mamelodi Sundowns, baada ya kutwaa mara ya kwanza 2016 ikiifunga Zamalek. wakihitimisha safari yao ya kishujaa barani Afrika kwa kubeba ndoo hiyo kubwa msimu huu!
👉 Endelea Kusoma na kutembelea sasa: thadeomedia5.blogspot.com

Maoni
Chapisha Maoni