𝐇𝐎𝐍𝐆𝐄𝐑𝐀 𝐏𝐎𝐋𝐈𝐒𝐈 𝐒𝐇𝐈𝐍𝐘𝐀𝐍𝐆𝐀 𝐊𝐔𝐃𝐇𝐈𝐁𝐈𝐓𝐈 𝐔𝐇𝐀𝐋𝐈𝐅𝐔 𝐍𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐋𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐀𝐌𝐀𝐍𝐈

Na, mwandishi wetu Shinyanga 

Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga imelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga chini ya uongozi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, kwa juhudi zake za kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha hali ya usalama pamoja na amani kwa wananchi.

Picha: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi akizungumza kuhusu juhudi za Jeshi la Polisi katika kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Amani, Mila na Desturi Mkoa wa Shinyanga, Shehe Balilusa Khamis, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo. Katika tukio hilo, alikuwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa dini, wazee wa kimila pamoja na Mkuu wa Machifu wa Mkoa wa Shinyanga.

Picha: Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Amani, Mila na Desturi Mkoa wa Shinyanga, Shehe Balilusa Khamis akilipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa kazi nzuri ya kudumisha amani na utulivu wa jamii.

Shehe Khamis amesema juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu zimechangia kurejesha utulivu na kuimarisha hali ya amani katika jamii.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa zisizo za kweli zinazoweza kuleta hofu au taharuki, na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Ameongeza kuwa umoja na mshikamano kati ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila pamoja na vyombo vya usalama ni nguzo muhimu katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya jamii.

Picha: Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Shinyanga, Mtemi Kidola wa II akitoa wito kwa vijana kuzingatia maadili mema na kuheshimu sheria za nchi ili kudumisha amani katika jamii.

Kwa upande wake, Mtemi Kidola wa II, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Shinyanga, ametoa wito kwa wazee na viongozi wa jamii kuendelea kuwakumbusha vijana kuzingatia maadili mema, kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Picha: Viongozi wa dini, wazee wa kimila pamoja na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga wakijadili masuala ya usalama, amani na mshikamano wa jamii katika kikao kilicholenga kupongeza juhudi za kudhibiti uhalifu mkoani humo.



Kwa pamoja, jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa dini na kimila ili kudumisha amani, usalama na mshikamano kwa maendeleo ya Mkoa wa Shinyanga.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

𝐁𝐑𝐄𝐀𝐊𝐈𝐍𝐆 𝐍𝐄𝐖𝐒: 𝐌𝐇𝐄. 𝐃𝐊𝐓. 𝐒𝐀𝐌𝐈𝐀 𝐀𝐌𝐄𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀 𝐔𝐓𝐄𝐔𝐙𝐈

BREAKING: RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI MBALIMBALI

𝐓𝐀𝐇𝐀𝐃𝐇𝐀𝐑𝐈: 𝐏𝐎𝐋𝐈𝐒𝐈 𝐖𝐀𝐊𝐀𝐍𝐔𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐕𝐔𝐌𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐅𝐔𝐍𝐙𝐈 𝐔𝐃𝐎𝐌 𝐊𝐔𝐖𝐀𝐖𝐀