𝐌𝐀𝐌𝐀 𝐖𝐀𝐉𝐀𝐖𝐀𝐙𝐈𝐓𝐎 𝐄𝐏𝐔𝐊𝐄𝐍𝐈 𝐒𝐀𝐅𝐀𝐑𝐈 𝐍𝐃𝐄𝐅𝐔 𝐌𝐊𝐈𝐊𝐀𝐑𝐈𝐁𝐈𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐅𝐔𝐍𝐆𝐔𝐀
Na, Thadeo Gelema
Wanawake wajawazito wametakiwa kuepuka safari ndefu za mabasi wanapokuwa karibu kujifungua ili kujiepusha na madhara yanayoweza kuhatarisha maisha yao pamoja na watoto wanaowatarajia.
![]() |
| Picha: Sajenti David Ndimila akitoa elimu kwa wasafiri kuhusu usalama wa mama wajawazito safarini. |
Elimu hiyo imetolewa na Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, alipokuwa akizungumza na wasafiri ndani ya Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa Shinyanga.
![]() |
| Picha: Elimu ya usalama barabarani ikiendelea kutolewa kwa wajawazito katika Stendi Kuu ya Mabasi Shinyanga |
Sajenti Ndimila amesema wanawake wajawazito wanaosafiri wakiwa karibu kujifungua hukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kujifungua ghafla ndani ya basi pasipo uwepo wa wakunga au vifaa tiba vya kumsaidia mama na mtoto.
![]() |
| Picha: Wanawake wajawazito wakishauriwa kuepuka safari ndefu wanapokaribia kujifungua. |
Aidha, amesema mashimo yaliyopo barabarani pamoja na mitikisiko ya mabasi vinaweza kuhatarisha afya ya mama mjamzito, huku kukaa muda mrefu bila kutembea kukiongeza hatari ya damu kuganda miguuni.

Pia, ameeleza kuwa baadhi ya wanawake wajawazito hukumbana na changamoto ya msongo wa mawazo na unyanyasaji wanapokuwa safarini, hasa pale mabasi yanapokuwa yamejaa na kulazimika kusimama au kukosa nafasi nzuri ya kukaa.

Kutokana na hali hiyo, Sajenti Ndimila amewataka wananchi kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi ya familia ili kusaidia kulinda afya na usalama wa mama mjamzito pamoja na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.
Sambamba na hilo, wanawake wajawazito wameshauriwa kutumia magari binafsi au usafiri wenye mazingira rafiki zaidi wanapokuwa karibu kujifungua ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakiwa safarini.
![]() |
| Picha: Elimu ya usalama barabarani inaendelea kutolewa kwa wananchi ili kulinda maisha ya wajawazito safarini. |
Kwa ujumla, elimu hiyo inalenga kulinda afya na usalama wa mama wajawazito pamoja na watoto wanaowatarajia kwa kuwashauri kuepuka safari ndefu wanapokaribia kujifungua.





Maoni
Chapisha Maoni