𝐊𝐈𝐃𝐀𝐓𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐍𝐄 𝐀𝐅𝐀𝐑𝐈𝐊𝐈 𝐃𝐔𝐍𝐈𝐀 𝐒𝐇𝐈𝐍𝐘𝐀𝐍𝐆𝐀

 
Shinyanga 

Mwanafunzi wa kidato cha nne anayefahamika kwa jina la Rebecka Boniphace Maganga (17), aliyekuwa akisoma katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga, amefariki dunia kwa tuhuma za kujinyonga ndani ya chumba alichokuwa akiishi.

Tukio hilo lilitokea Aprili 27, 2026 majira ya saa saba mchana katika eneo la Old Shinyanga, ambapo inadaiwa mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kutumia mkanda wa sketi ya shule.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi Janeth Magomi, jeshi la polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa mlezi wa marehemu, Mashala Piter (56), ambaye aligundua tukio hilo.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa tukio hilo linaweza kuhusishwa na msongo wa mawazo, baada ya mwanafunzi huyo kurejeshwa nyumbani na mwalimu wake akiwa na mzazi wake kufuatia kutohudhuria masomo kwa muda wa wiki mbili bila taarifa.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Senyenge, kijiji cha Old Shinyanga, Benjamin Andrew, alisema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa sita mchana na walipofika eneo la tukio walimkuta mwanafunzi huyo tayari amefariki dunia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Manispaa ya Shinyanga, Bi. Meryester Nyalusanda, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kubaini mapema changamoto wanazopitia.

Alisema ni muhimu familia kuwa na mawasiliano ya karibu ili kusaidia watoto kukabiliana na changamoto za kisaikolojia badala ya kuchukua hatua kali kabla ya kuelewa tatizo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa uchunguzi zaidi, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

🔚 Kwa ujumla, Tukio hili linaibua haja ya jamii, hasa wazazi na walezi, kuimarisha mawasiliano na watoto ili kubaini mapema changamoto za kisaikolojia wanazopitia. Ushirikiano kati ya familia, shule na jamii ni muhimu katika kulinda afya ya akili ya vijana na kuzuia matukio kama haya yasijirudie.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

𝐉𝐄, 𝐖𝐀𝐉𝐔𝐀? 𝐋𝐈𝐌𝐀𝐎 𝐍𝐈 𝐓𝐔𝐍𝐃𝐀 𝐀𝐔 𝐊𝐈𝐔𝐍𝐆𝐎!

𝐆𝐀𝐌𝐎𝐍𝐃𝐈; 𝐀𝐓𝐀𝐍𝐆𝐀𝐙𝐀 𝐊𝐈𝐊𝐎𝐒𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐒𝐓𝐀𝐑𝐒