MSAKO WAANZA: POLISI ARUSHA MAUAJI YA MFANYABIASHARA WA MADINI
Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watu wanaohusishwa na mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Abdillah Musa Mollel maarufu kama Banjo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa, Februari 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, amesema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na linahitaji ushirikiano wa jamii ili kuwabaini wahusika.
Kamanda Masejo ameeleza kuwa Februari 13, 2026 Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kupotea kwa mfanyabiashara huyo, ndipo msako na uchunguzi ulipoanza mara moja. Amedai kuwa wakati uchunguzi ukiendelea, Februari 19, 2026 walipokea taarifa za kuonekana kwa mwili wa marehemu katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ukiwa tayari umefariki.
Marehemu Banjo, ambaye alikuwa akiishi katika eneo la Sanawari jijini Arusha, inadaiwa alionekana kwa mara ya mwisho hadharani alipokuwa akifanya mazoezi ya mwili katika jengo moja katikati ya Jiji la Arusha. Mwili wake umewasili mkoani Arusha na taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake Sanawari.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika.
Kwa ujumla, Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kufanikisha kukamatwa kwa wahusika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na haki itendeke.
Maoni
Chapisha Maoni