MAPYA YAIBUKA MANGUNGU SIMBA KUANZA UTOAJI KADI ZA UANACHAMA MACHI 27, 2026
Hii ni Thadeo Media
Leo Februari 10, 2026 Klabu ya Simba SC imetangaza kuingia mkataba rasmi na kampuni za Mainstream Group na Nexus Pesa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la utoaji wa kadi mpya za uanachama, hatua inayolenga kuhuisha mfumo wa uanachama wa klabu hiyo kongwe nchini.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi na Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu, amesema kuwa utoaji wa kadi hizo utafanyika kwa kuzingatia kikamilifu katiba ya klabu, kuanzia ngazi ya matawi hadi makao makuu ya klabu.
Mangungu amebainisha kuwa muda uliopo sasa ni muafaka hasa kwa wanachama waliopo kwenye matawi, huku akithibitisha kuwa zoezi la usajili wa matawi litaanza hivi karibuni kama sehemu ya maandalizi ya utoaji wa kadi hizo.
“Klabu imepanga kuanza rasmi kutoa kadi za uanachama tarehe 27 Machi, 2026. Maandalizi haya yanahusisha taasisi mbalimbali, hivyo tumelazimika kuchukua muda ili kuhakikisha zoezi linafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zote,” amesema Mangungu.
Ameongeza kuwa zoezi hilo lina manufaa makubwa kwa klabu, ikiwemo kuwasaidia wanachama waliopoteza kadi zao kuzipata upya, kuwahudumia wale waliokuwa hawajawahi kupata kadi, pamoja na kuboresha taarifa na kumbukumbu sahihi za wanachama wa klabu.
“Kupitia zoezi hili, tutaweza kuwa na rekodi sahihi na za kisasa za wanachama wetu, jambo litakalotusaidia katika mipango ya maendeleo na uendeshaji wa klabu,” amesisitiza.Murtaza Mangungu akieleza mpango wa uwekezaji na kuanza utoaji wa kadi mpya za uanachama wa Simba SC kuanzia 27 Machi 2026.
Aidha, Mangungu amesema kuwa utaratibu wa kupata kadi hizo utaendelea kuwa kama ulivyokuwa awali, ambapo maombi yote ya uanachama yatawasilishwa kupitia matawi. Pia, Simba SC imepanga kuwa na matawi maalum kwa wanachama waliopo nje ya nchi ili kuwahusisha kikamilifu katika mfumo mpya wa uanachama.
Maoni
Chapisha Maoni