CRISTIANO RONALDO AREJEA MAZOEZINI AL NASSR BAADA YA KUMALIZA MGOMO

Picha:Nyota wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo. Picha na Mtandao

Hii ni Thadeo Media 

Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ureno na nyota wa klabu ya Al Nassr, Cristiano Ronaldo, amehitimisha rasmi mgomo wake wa mechi kadhaa na kurejea katika mazoezi ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

Ronaldo alikuwa amekosa mechi mbili mfululizo baada ya kuibuka kwa sintofahamu ndani ya klabu hiyo, hali iliyotajwa kusababishwa na kutoridhishwa kwake na baadhi ya mambo ya kiuendeshaji yanayoendelea Al Nassr.

Taarifa zinaeleza kuwa mchezaji huyo nguli alikerwa na changamoto za kifedha zinazoikumba klabu hiyo, hali ambayo imeathiri hata juhudi za usajili wa wachezaji wapya ili kuimarisha kikosi. Changamoto hizo zimedaiwa kusababisha sintofahamu kati ya uongozi wa klabu na baadhi ya wachezaji wakubwa.

Aidha, Ronaldo pia alionesha kutoridhishwa na hatua ya hasimu wao mkubwa, Al Hilal, kumsajili mshambuliaji Karim Benzema, aliyewahi kuwa mchezaji mwenzake kwa miaka kadhaa walipokuwa wakiichezea klabu ya Real Madrid nchini Hispania.

Mbali na hilo, mgomo huo umehusishwa pia na madai ya kuwepo kwa ukosefu wa usawa ndani ya klabu ya Al Nassr, hususan suala la kucheleweshwa kwa mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi wa klabu hiyo mara kadhaa, hali iliyodaiwa kumuudhi mchezaji huyo mwenye ushawishi mkubwa.

Baada ya kurejea mazoezini, Ronaldo sasa anatarajiwa kurejea uwanjani na kuiongoza Al Nassr katika mchezo ujao wa ligi dhidi ya Al Fateh, utakaopigwa Jumamosi.

Ronaldo anatarajiwa kurejea uwanjani Jumamosi Februari 14, 2026 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Al-Fateh. Picha na Mtandao
Kwa upande wa mafanikio binafsi, Cristiano Ronaldo ameendelea kuandika historia katika soka la dunia baada ya kufikisha jumla ya mabao 961 katika maisha yake ya soka ya klabu na timu ya taifa, akibakiza hatua chache tu kufikia rekodi ya kihistoria ya mabao 1000.

Kwa ujumla, Kurejea kwa Cristiano Ronaldo mazoezini ni ishara ya kurejea kwa utulivu ndani ya Al Nassr na kunatoa matumaini mapya kwa mashabiki wa klabu hiyo. Matarajio sasa yanaelekezwa katika mchango wake uwanjani, huku dunia ya soka ikiendelea kushuhudia safari yake ya kihistoria kuelekea kufikisha mabao 1000.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

𝐉𝐄, 𝐖𝐀𝐉𝐔𝐀? 𝐋𝐈𝐌𝐀𝐎 𝐍𝐈 𝐓𝐔𝐍𝐃𝐀 𝐀𝐔 𝐊𝐈𝐔𝐍𝐆𝐎!

𝐆𝐀𝐌𝐎𝐍𝐃𝐈; 𝐀𝐓𝐀𝐍𝐆𝐀𝐙𝐀 𝐊𝐈𝐊𝐎𝐒𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐒𝐓𝐀𝐑𝐒