HUU NI WAKATI WA VIJANA KUACHA KUONA SEKTA YA MADINI KAMA YA WENYE MITAJI MIKUBWA PEKEE
Hii ni Thadeo Media
Sekta ya madini nchini imepiga hatua kubwa ya kihistoria baada ya Tanzania kuingia rasmi katika orodha ya mataifa yenye akiba kubwa ya madini barani Afrika, hatua inayotajwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa taifa, uzalishaji wa ajira na kuongezeka kwa fursa za kiubunifu kwa vijana.
Akizungumza jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio ya siku 100 za kwanza za kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tanzania imefanikiwa kununua tani 17 za dhahabu ndani ya siku 100 pekee. Hatua hiyo imeimarisha akiba ya taifa na kuongeza mchango wa sekta ya madini kutoka asilimia 10.1 hadi asilimia 11.2 ya Pato la Taifa.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na sera thabiti za serikali zinazovutia uwekezaji wa ndani na nje, hususan katika ujenzi wa viwanda vya kusafisha na kuyeyusha madini ndani ya nchi. Hatua ya kuachana na utaratibu wa kusafirisha madini ghafi imefungua milango mipya ya ajira kwa vijana katika viwanda vya kisasa vinavyojengwa nchini.
Waziri Mavunde amesema sekta ya madini kwa sasa haihitaji tu wachimbaji, bali pia vijana wenye ujuzi wa teknolojia, ubunifu wa kidijitali na maarifa ya kiufundi katika uendeshaji wa viwanda. Amehimiza vijana kuacha kuiona sekta hiyo kama ya watu wenye mitaji mikubwa pekee, na badala yake kuitazama kama fursa ya kutumia maarifa na ubunifu wao kujiajiri na kuongeza thamani ya rasilimali za taifa.
Serikali imesisitiza kuwa mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo sasa yanalenga kuhakikisha madini yanabaki nchini kwa kiwango kikubwa ili kukuza mzunguko wa fedha, kuimarisha thamani ya sarafu ya nchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii.
Kwa ujumla, Hatua ya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye akiba kubwa ya dhahabu imetajwa kuwa uthibitisho kuwa zama za kuuza rasilimali bila faida zimepitwa na wakati, na sasa ni kipindi cha uwekezaji wenye tija unaojali matumizi ya nguvu kazi ya ndani na mustakabali wa vizazi vijavyo kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.
Maoni
Chapisha Maoni