Habari
SERIKALI YAJIANDAA KUIMARISHA UMOJA WA TAIFA KUPITIA TUME YA MARIDHIANO 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuwa Serikali imeanza rasmi mchakato wa kuunda Tume ya Maridhiano kama sehemu ya mkakati wa kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa kuelekea mwaka 2026.
Akizungumza katika hotuba yake ya kuaga mwaka 2025 leo 31, Desemba 2025 na kuukaribisha mwaka 2026 iliyotolewa Ikulu Zanzibar, Rais Samia amesema Serikali imepanga kuanza mwaka mpya kwa kuimarisha mshikamano wa kitaifa, ambapo maandalizi ya kuunda tume hiyo tayari yameanza. Amesisitiza kuwa Serikali itashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali ili kufikia makubaliano kuhusu muundo wa tume hiyo.
Rais Samia amebainisha kuwa mwaka 2025 ulikuwa na mafanikio pamoja na changamoto zilizohitaji subira, mshikamano na uzalendo wa hali ya juu. Akitaja matukio ya mwezi Oktoba, Rais amesema nchi ilipitia nyakati ngumu zilizohitaji umoja wa dhati kutoka kwa Watanzania wote.
“Ninavishukuru vyombo vyetu vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa letu,” amesema Rais Samia, akiongeza kuwa Tanzania imeendelea kuthibitisha kwa ulimwengu kuwa ni taifa imara, linalostahimili changamoto na lenye uwezo wa kujitathmini na kujirekebisha.
Katika kuanza mwaka 2026, Rais Samia amesema Serikali itahakikisha inashirikiana na wadau wote katika kujadili muundo wa Tume ya Maridhiano, ikiwemo aina ya wajumbe watakaounda tume hiyo, majukumu yao pamoja na muda wa utekelezaji wa kazi za tume.
Hatua ya kuanza mchakato wa kuunda Tume ya Maridhiano inaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha umoja wa kitaifa kwa njia ya mazungumzo, ushirikishwaji na maridhiano. Ushirikiano wa wadau wote utakuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia kudumisha amani, mshikamano na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Maoni
Chapisha Maoni