Siasa
Ahmed Salum Aliongoza Kura za Maoni CCM Jimbo la Solwa
Na Mwandishi Wetu – Thadeo Gelema, Agosti 5
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Solwa, Ahmed Ally Salum, aliongoza kwa kishindo kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika tarehe 4 Agosti 2025 katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini.
Katika kura hizo, Salum alipata kura 3,862 kati ya kura halali 7,012 zilizopigwa, huku hakuna kura iliyoharibika. Aliongoza kwa tofauti kubwa dhidi ya wagombea wengine sita waliokuwa wakichuana naye kwenye mchakato huo wa ndani ya chama.
Aliyeshika nafasi ya pili alikuwa Sosthenes Julius Katwale aliyepata kura 2,288. Wengine waliopata kura ni Selemani Emmanuel Chokala (645), Zinguji Mayala Machwele (67), Alphistone Michael Bushi (61), Costantine Joseph Budaga (59), na Leonard Nduta Lukanya aliyepata kura 30 pekee.
Matokeo hayo yalitangazwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bi Erenestina Richard. Hata hivyo, alifafanua kuwa ushindi huo si uteuzi rasmi wa mgombea.
“Haya ni matokeo ya awali ya kura za maoni. Kuongoza hapa hakumaanishi tayari umeteuliwa. Tunawaomba wagombea wote kuwa watulivu wakisubiri uamuzi wa vikao vya juu vya chama,” alisema Erenestina.
Wanachama wa CCM waliojitokeza kushiriki kura hizo walionesha hamasa kubwa, jambo linalodhihirisha nguvu ya demokrasia ya ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Endelea kufuatilia Thadeo Media kwa taarifa zaidi
Maoni
Chapisha Maoni