SMAUJATA WAOKOA MTOTO WA MIAKA 10 MSALALA

Kahama, Shinyanga

Kwa mjibu wa Misalaba media blog Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Halmashauri ya Msalala, Bi. Nives Nyoni, aliiongoza operesheni ya kumwokoa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10 aliyedaiwa kufanyiwa ukatili na mama yake mzazi katika kijiji cha Isaka Station, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

PICHA CHANZO: Misalaba Media Blog



Tukio hilo lilitokea Aprili 23, 2026 majira ya saa mbili usiku, ambapo mtoto huyo alikimbilia nyumbani kwa Bi. Nyoni kuomba msaada, akieleza kuwa alikuwa akipigwa mara kwa mara, alinyimwa haki ya kwenda shule na kufanyiwa vitendo vya mateso.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bi. Nyoni alimhifadhi mtoto huyo kwa muda na aliwasiliana na viongozi wa SMAUJATA, akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Nabila Kisendi, kwa ajili ya hatua zaidi za uokoaji.

Asubuhi iliyofuata, kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Msalala pamoja na Jeshi la Polisi, mtoto huyo alipelekwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi na hatua za kisheria dhidi ya mzazi aliyekuwa akituhumiwa.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mama mzazi wa mtoto huyo alikuwa na changamoto ya afya ya akili, hali iliyosababisha mamlaka husika kuchukua uamuzi wa kumkabidhi mtoto huyo kwa baba yake mzazi anayeishi Misungwi mkoani Mwanza.

Viongozi wa SMAUJATA pamoja na maafisa wa serikali za eneo hilo walisema wataendelea kufuatilia ustawi wa mtoto huyo hata baada ya kuhamishiwa kwa baba yake.

PICHA CHANZO: Misalaba Media Blog

🔚 kwa ujumla, Tukio hilo lilionesha umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii, taasisi za kijamii na vyombo vya dola katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili. Pia lilisisitiza haja ya wazazi na walezi kuwapatia watoto malezi bora, salama na yenye haki ya elimu.

Maoni